Vipengele gani vya kuzingatia ili wanaotaka kufunga ndoa wakubaliwe kisheria kufunga ndoa
(a) Ni lazima muungano uwe wa hiari
Mume na mke wawe wameamua kuishi pamoja kwa ridhaa yao wenyewe. Hii inamaanisha kusiwe na kulazimishwa, kuhadaiwa kwa aina yoyote kwani muungano kama huo utakuwa batili kisheria.
Ni kosa la jinai kushiriki katika shughuli ya ndoa ambayo mmoja wapo au wote wamelazimishwa kufunga ndoa.
(b) Muungano uwe ni kati ya mwanamke na mwanamme
Muungano wa watu wa jinsia moja hata kama ni wa hiari muungano huo hautambuliki kisheria. Pia mtu huhesabika mwanamke au mwanamme kutokana na
sehemu za siri alizozaliwa nazo na siyo alizozipata baadaye.
Jamii inachukulia kuwa ndoa ni njia pekee ya kujipanua, upanukaji huku ni kwa kuzaa watoto.
Kwa hali hiyo ili kupata watoto ni lazima ndoa iwe kati ya mwanamme na mwanamke.
(c) Muungano huo uwe unakusudiwa kuwa wa kudumu
Pamoja na kuwa mwanamke na mwanamme wameamua kuishi pamoja kwa hiari yao lakini siyo kwa kutodumu muungano huo hautambuliki kisheria kama ndoa.
Muungano ni lazima uwe wa kudumu
maisha yote au kama mmoja wao amefariki au kama ndoa imekumbwa na matatizo na mahakama ikaona ni bora kutoa talaka kwa yeyote aliyefika kulalamika.
(d) Wanandoa wasiwe maharimu
Maharimu ni watu walio na mahusiano ya karibu ya damu au kindugu.
Wawili wanaoamua kufunga ndoa wasiwe na uhusiano wa karibu kindugu.
Inakatazwa katika kifungu cha 14 cha Sheria ya ndoa ya mwaka
1971 mtu kuoa au kuolewa na mzazi wake, mtoto au mjukuu wake, kama ni dada yake, mama aushangazi au baba wa mjomba wake, baba au mama wa kambo na mwanaye aliyemfanya kuwa mtoto
wake (adopted child).
(e) Wanandoa wawe wametimiza umri unaokubalika kisheria
Mwanamke na mwanamme wawe wametimiza miaka 18 ili kufunga ndoa.
Hata hivyo mwanamke anaweza kuolewa akiwa na umri wa chini ya miaka18 lakini sio chini ya miaka 15 kama atapata idhini ambayo hutolewa na baba na kama hayupo ni mama au kama wote wamefariki idhini itatolewa na mlezi wa binti huyo.
Kama wote wamefariki basi hatahitaji idhini.
Kuna wakati katika mazingira fulani
mahakama inaweza kutoa idhini kwa binti kuolewa akiwa na miaka 14 lakini si chini ya hapo ikiwaataonekana kwa mfano ana mimba.
Pia mwanaume anaweza kuruhusiwa na mahakama kuoa akiwa na umri wa miaka chini ya 18 lakini lakini si chini ya 16
kama ataonyesha kuelewa jukumu lake kama mtu mzima.
Lakini hii ni pale ambapo kuna tatizo kama la kumpa msichana mimba ndipo mahakama inaweza
ikatoa idhini.
Hii inathibitishwa katika ombi la kuoa la Shabiri A. M Virji (1971) HCD no.407 la Mahakama Kuu ya Tanzania, mwombaji alikuwa na miaka 16 lakini
alimpa mimba binti wa miaka 18.
Mahakama katika kuchunguza ombi la mvulana la kuoa ilitoa kibali kwa
sababu wote wawili walipendana sana na wazazi wao hawakuwa na kipingamizi cha wao kuoana.
(f) Kusiwe na ndoa inayoendelea
Kama mwanamke ana ndoa inayoendelea na
inatambulika kisheria haruhusiwi kufunga ndoa nyingine (polyandry).
Kadhalika kama mwanamme
ana ndoa ya mke mmoja au kama ni mwislamu ana wake wanne tayari hataruhusiwa kufunga tena
ndoa.
(g) Kusiwe na kipingamizi
Kama ndoa imezuiwa na Mahakama au halmashauri ya usuluhishi kutokana na uwezo zilizopewa na ndoa ikaendelea kufungwa kabla ya wenye
kupeleka kipingamizi hawajasikilizwa au Mahakama imeshaamua ndoa hiyo isifungwe basi ndoa hiyo
itakuwa ni batili.
(h) Mfungishaji ndoa kutokuwa na mamlaka
Kama wanaofunga ndoa wanajua wazi kuwa
anayewafungisha ndoa hana mamlaka hayo na kwa makusudu wakakubali awafungishe ndoa basi ndoa hiyo itakuwa ni batili.
Mfungishaji ndoa ili kuwa na
mamlaka anapaswa kusajiliwa na Msajili Mkuu wa Ndoa na kupewa leseni ya kufungisha ndoa.
(i) Kutokuwepo kwa wafunga ndoa
Kama ndoa imefungwa bila ya wafunga ndoa wote kuwepo basi ndoa hiyo haitambukuliwa kisheria.
Hata hivyo sheria inaruhusu ndoa kufungwa ikiwa mmoja
wa wafunga ndoa hayupo, kama mfunga ndoa ambaye hayupo amewakilishwa na mtu ambaye alikuwepo wakati mfunga ndoa hayupo, alipotoa ridhaa yake ya kuoa au kuolewa.
(j) Mashahidi wa ndoa
Ili ndoa itambulike kisheria ni lazima ishuhudiwe na mashahidi wasiopungua wawili ambao wanaruhusiwa
kisheria yaani umri wao usipungue miaka 18 na wafahamu kinachosemwa na kutendeka wakati wa kufunga ndoa.
(k) Kuwa katika eda
Eda ni kipindi cha kukaa ndani kinachotolewa kwa mwanamke wa kiislamu aliyeachika katika ndoa au aliyefiwa na mumewe, ili taratibu fulani za kidini
zifanyike.
Kama mwanamke ambaye ndoa ilifungwa kiislamu anaolewa wakati wa kipindi cha eda hakijaisha basi ndoa hiyo itakuwa batili.
Lakini mfaruku hiyo ni pale iwapo mtalikiwa awe anafuata dini ya Kiislamu.
Kama atabadili dini baada ya kufiwa au kupewa talaka masharti ya eda
hayatambana na atakuwa huru kuolewa.
Aina za ufungaji ndoa na taratibu za kufuata
Taarifa ya nia ya kuoa
Kwanza kama mwanamke na mwanamme wanataka kufunga ndoa ni wajibu taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe kwa mfungishaji ndoa siku 21 kabla ya
siku ya kufunga ndoa.
Taarifa hiyo ionyeshe mambo yafuatayo:-
(i) Majina kamili na umri wa wanaotaka
kuoana.
(ii) Uthibitisho kwamba hakuna kipingamizi
dhidi ya hiyo ndoa wanayotarajia kufunga.
(iii) Majina kamili ya wazazi wao na sehemu
wanakoishi.
(iv) Hadhi ya wafunga ndoa, yaani kama ni mwanamke ifahamike kama hajaolewa,
ametalakiwa au ni mjane na mwanamme pia anapaswa kama hajaoa, au ana mke au/wake wengine (hii ni kwa ndoa za kiserikali na kiislamuu) au kama ametaliki.
(v)Kama muolewaji ana umri chini ya miaka 18, jina la mtu aliyetoa idhini ya yeye kuolewa kama yupo ionyeshwe.
(vi) Kama ni ndoa ya kiserikali au kiislamuu hapana budi kueleza kama ndoa ni ya wake wengi au inatazamiwa kuwa ya wake wengi, majina ya wake waliopo yatajwe.
Pia katika fungu hili kama mtu anataka ndoa iwe ya mke mmoja anapaswa kueleza.
Baada ya taarifa yenye maelezo haya kufikishwa kwa mfungishaji ndoa yeye anawajibika kutangaza hii nia ya kufunga ndoa.
Sababu ya kufanya hivyo ni ili kama kuna mwenye kipinganizi na ndoa hiyo atoe taarifa.
Matangazo haya hutolewa kama ndoa inatarajiwa kufungwa kidini, sehemu za ibada.
Kama ni ndoa ya kiserikali tangazo litabandikwa nje ya ofisi ya msajili wa Ndoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya.
Vipingamizi vya ndoa viko vya aina mbili, cha kwanza ni kile cha kisheria yaani kama ndoa itakayofungwa itakuwa batili.
Kipingamizi cha pili ni kama muoaji ana mke au wake wengine tayari, hivyo mke au wake wanaweza kutoa kipingamizi kama uwezo wa muoaji kifedha ni mdogo kiasi kwamba kuongeza mke mwingine kutazidisha shida.
Mfungishaji ndoa anapopokea taarifa ya kupinga ndoa isifungwe, ataipeleka taarifa hiyo kwenye Baraza la Usuluhishi la Ndoa.
Huko aliyewekewa kipingamizi na aliyeweka wataitwa na kila mmoja
atajieleza.
Baada ya kusikiliza pande zote Baraza
lina uwezo wa kuamua ndoa hiyo ifungwe au isifungwe na mfungishaji ndoa atafuata uamuzi wa Baraza.
Kama mtu atatoa kipingamizi cha uongo na ikithibitika hivyo, adhabu yake anaweza kufungwa kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Baada ya kipengele hiki kutimizwa ndoa inaweza kufungwa.
Comments
Post a Comment