ENVIRONMENTAL MANAGEMENT ACT
MAELEZO YA KIFUPI KUHUSU SHERIA YA MAZINGIRA YA MWAKA 2004
Sehemu ya kwanza Sheria ya Mazingira ya
Mwaka 2004 ambayo inakusudia kuweka muundo wa kisheria na taasisi
utakaoweka usimamizi endelevu ya mazingira katika kutekeleza Sera ya
Taifa ya Mazingira. Muswada huu unaainisha misingi ya usimamizi wa
mazingira kama vile Kanuni ya msingi ya haja ya kuchukua tahadhari
panapokuwa na wasiwasi kuwa shughuli inayotaka kufanyika itakuwa na
madhara kwa mazingira; basi isifanyike hata kama hakuna ushahidi wa
kisayansi. Kanuni nyingine ya msingi ni ya mchafuzi kuwajibika kulipa
gharama za kusafisha uchavuzi au kurekebisha uharibifu alioufanya.
Sehemu hii pia ina kanuni ya msingi juu ya ushirikishwaji wa jamii katika
utayarishaji wa sera, mipango na michakato ya usimamizi na hifadhi ya
mazingira
Sehemu ya Pili ina misingi mikuu inayotumika katika usimamizi
wa mazingira pamoja na wajibu wa kulinda mazingira. Sehemu
inapendekeza vifungu vya sheria vitakavyohakikisha haki kwa kila mtu
aliyepo Tanzania kuishi katika mazingira safi, salama na yanayolinda afya.
Haki ya kuishi katika mazingira safi, salama na yanayolinda afya
inajumuisha pia haki ya kila raia kutumia Mazingira kwa ajili ya shughuli
za burudani, starehe, elimu, afya, dini, utamaduni na uchumi. .
Sehemu ya Tatu inahusu mfumo wa kitaasisi na utawala katika
utekelezaji wa sheria inayopendekezwa. Hi inajumuisha uundwaji na
uainishaji wa majukumu ya Waziri, Kamati ya Taifa ya Ushauri kuhusu
Masuala ya Mazingira, Mkurugenzi wa Mazingira, Baraza la Taifa la
Usimamizi wa mazingira, wizara na sekta mbalimbali, sekretarieti ya
mkoa pamoja na ngazi zote za serikali za mitaa.
Schemu ya Nne ina vifungu juu ya utayarishaji na utekelezaji wa
mipango inayozingatia masuala ya mazingira ambayo itapaswa kuzingatia
dharura ambazo zinaweze kutokea katika Mazingira. Sehemu hii ina
vifungu juu ya mipango ya masuala ya mazingira katika ngazi ya serikali
za mitaa, ngazi ya sekta ngazi ya taifa.
Sehemu ya Tano, ambayo inahusu usimamizi wa mazingira
inaweka vifungu vinavyojumuisha masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na
uanzishaji wa maeneo ya kipekee ya mazingira yanayohitaji hifadhi nje ya
maeneo mengine ya hifadhi ya kitaifa. Sehemu hii pia ina vifungu juu ya
mipango ya usimamizi wa mazingira kwa maeneo ya hifadhi kitaifa
pamoja na ulinzi wake. Sehemu hii inatoa pia masharti juu ya hifadhi ya
maeneo nyeti kimazingira, kingo za mito, bahari na fukwe zake, maziwana fukwe zake, ardhioevu, milima, mandhari, hifadhi ya bioanuwai,
matumizi ya rasilimali za kigenetiki za Tanzania pamoja na usimamizi na
uingizaji nchini wa vinasaba vilivyofanyiwa mabadiliko ya kigenetiki na
mazao yake. Pia sehemu hii inaweka masharti yanayohusu hifadhi ya
urithi wa kiutamaduni, hifadhi ya usafi wa anga na mabadiliko ya
tabia nchi.
Sehemu ya Sita inahusu tathimini ya athari kwa mazingira ambayo
inatambulika kimataifa na kuwa sehemu muhimu katika mikataba ya
kimataifa ya mazingira kama nyenzo muhimu ya utatatibu wa uchambuzi,
ambao hufanyika i1i kufahamu kama programu, shughuli au mradi utakuwa
na athari kubwa kwenye mazingira na namna ya kuiepuka. Sehemu hii pia
inatoa masharti kwa miradi au shughuli zitakazohitaji kufanyiwa tathimini
ya athari kwa mazingira kabla ya kuanza kutekelezwa. Hayo ni pamoja na
sharti kuwa tathimini hiyo itafanywa na wataalamu au kampuni ya
wataalam iliyoandikishwa katika daftari maalum ambao wataruhusiwa
kufanya shughuli hiyo nchini.
Sehemu ya Saba inaweka masharti juu ya nyenzo mpya ya kisheria
juu ya tathimini ya athari kimkakati kwa mazingira ambayo inataka
miswada ya sheria, sera, mipango na programu mbalimbali za serikali na
taasisi zake inapopendekezwa maelezo ya kina yatolewe i1i tathimini
ifanyike kuona kama utekelezaji wake hautakuwa na athari kwa mazingira
na matumizi endelevu ya mali asili.
Sehemu ya Nane inatoa masharti juu ya hatua za kuchukuliwa za
kuzuia uchafuzi wa mazingira na udhibiti wa uchafu huo pindi unapotokea.
Sehemu hii ina vifungu vya kina vinavyohusu uchafuzi wa mazingira na
uwezo wa Waziri kutengeneza kanuni za kuzuia na kudhibiti uchafuzi huo.
Sehemu hii, pamoja na mambo mengine, inazuia uchafuzi wa maji, utupaji
wa vitu vya hatari venye sumu, kemikali na umwagaji wa mafuta kwenye
mazingira, pamoja na uzuiaji wa shughuli na michakato ambayo ni hatari
kwa mazingira.
Sehemu ya Tisa inahusu usimamizi wa taka. Sehemu hii
inatenganisha kwa makusudi masharti yanayohusu usimamizi na utupaji wa taka ngumu; uzuiaji wa utupaji hovyo wa taka taka katika maeneo ya
wazi na majumbani; utupaji na usafirishaji wa maji taka; uzuiaji wa
uchafuzi wa hewa; na utupaji wa takataka zenye sumu. Sehemu hii inazipa
serikali za mitaa jukumu maalum la kupunguza taka ngumu, maji taka,
uchafuzi wa hewa na takataka zenye sumu katika maeneo yao
Sehemu ya Kumi. Sehemu hii inatambua umuhimu
wa nafasi ya Kamati ya Kitaifa ya Viwango vya Ubora wa Mazingira chini
ya Shirika la Viwango Tanzania. Kamati hii ina wajibu wa kuangalia
maendeleo pamoja na kupitia na kukusanya mapendekezo ya kuwekwa
viwango na kuviwasilisha kwa Waziri ili avitangaze kuwa viwango vya
kitaifa. Kila mtu anayefanya shughuli yoyote inayogusa masuala ya
mazingira atatakiwa kuheshimu na kutekeleza masharti ya viwango vya
ubora wa mazingira vilivyowekwa.
Sehemu ya Kumi na Moja inaweka amri juu ya urudishaji wa hali
ya mazingira katika hali yake ya awali, amri ya kupewa njia ya kupita na
kuingia katika eneo linalohitaji hifadhi ya mazingira na amri ya kuhifadhi
mazingira. Amri ya kurudisha mazingira katika hali yake ya awali na
kuhakikisha mtu ambaye ameharibu mazingira anawajibika kuyarudisha
katika hali yake kwa kadri itakavyowezekana kama ilivyokuwa mwanzo
kabla ya kuharibiwa inatolewa hasa katika shughuli za uchimbaji madini.
Amri ya kupewa njia ya kupita na kuingia katika eneo linalohitaji hifadhi
ya mazingira inatolewa kwenye ardhi ambayo imewekewa masharti ya
kutunzwa ili kuhifadhi mazingira.
Sehemu ya Kumi na Mbili inayoshughulikia uchanganuzi na
kumbukumbu ina vifungu juu ya uteuzi wa maabara, wataalam wa
uchanganuzi na mabingwa wa uchanganuzi kwa ajili ya uchukuaji wa sampuli na uchanganuzi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa pamoja na mambo
mengine viwango vya ubora wa mazingira, unafuatwa na kutiliwa nguvu.
Sehemu hii pia ina vifungu vya uwasilishaji wa kumbukumbu na taarifa
kutoka taasisi mbalimbali juu ya athari kwa mazingira. Baraza la Taifa la
Hifadhi ya Mazingira linatakiwa kutunza kumbukumbu zote kwa
kuzingatia masharti ya utunzaji wa siri kwa mujibu wa sheria.
Sehemu ya Kumi na Tatu inahakikisha uhuru wa kila raia kupata
habari juu ya mazingira kwa mujibu wa sheria. Sehemu hii pia inatoa kwa
Mkurugenzi wa Mazingira na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza haki ya kupata
taarifa na habari za mazingira kutoka kwa mtu yeyote zitakazowawezesha
kutimiza wajibu na majukumu yao. Sehemu hii ina kifungu juu ya
kuanzishwa kwa chombo kikuu cha kukusanya taarifa za mazingira ikiwa
ni pamoja na takwimu zilizotolewa na vyombo vya umma au binafsi katika
utunzaji na usimamizi wa mazingira. Utafiti wa mazingira pamoja na
elimu ya mazingira na uelimishaji wa umma yameelezwa katika sehemu
hii. Mkurugenzi wa Mazingira anatakiwa chini ya sheria hii kutayarisha
na kutangaza kila baada ya miaka miwili taarifa ya hali ya mazingira
ambayo pia itawasilishwa Bungeni kwa taarifa.
Sehemu ya Kumi na Nne inahusu ushirikishwaji wa Umma katika
utoaji wa maamuzi juu ya masuala ya mazingira kama yalivyoelekezwa
katika Msingi wa Kumi ya Azimio la Rio. Ushirikishwaji wa umma katika
Sehemu hauishii tu katika ushiriki kwenye masuala ya tathimini ya athari
kwa mazingira bali pia katika nyanja nyingine za maamuzi. Katika
sehemu hii wananchi wanahakikishiwa haki yao ya kushiriki na kutoa
maamuzi juu ya utengenezaji wa sera ya mazingira, malengo, mipango na
kuwashirikisha katika utayarishaji wa sheria na kanuni zinazohusu
mazingira.
Sehemu ya Kumi na Tano ya Muswada huu inahusu mikataba ya
kimataifa inayohusu mambo ya usimamizi na udhibiti wa mazingira.
Sehemu hii pia inazungumzia juu ya uandaaji wa mapendekezo ya kisheria
juu ya utekelezaji wa mikataba hiyo. Pia inahusu haja ya kuanzishwa kwa
mazungumzo na nchi jirani juu ya uanzishaji wa programu za usimamizi
wa mazingira kwa ajili ya kuondoa na kupunguza uharibifu wa mazingiraunaoweza kutokea katika maeneo yanayovuka mipaka lakini
yanayoshabihiana kimazingira.
Sehemu ya Kumi na Sita ina vifungu juu ya kuheshimu na kufuata
sheria ikiwa ni pamoja na masuala ya hima sheria. Pia inaelezea uteuzi wa
wakaguzi wa mazingira, kazi zao na utendeshaji wa kesi mbalimbali
unaofanywa na wakaguzi hao. Aidha inaelezea uteuzi wa wakaguzi wa
mazingira kutoka katika taasisi na ofisi mbalimbali za serikali. Wakaguzi
hao wa mazingira wanaweza kuteuliwa kutoka Baraza, serikali za mitaa au
taasisi yoyote ya umma. Uteuzi huo unaweza kufanywa kwa kutamka jina
la mtu au la taasisi. Sehemu hii pia inazungumzia makosa mbalimbali juu
ya uharibifu wa mazingira na adhabu zake. Sehemu hii inatoa mamlaka ya
kutoa amri kwa mtu yeyote ili kuzuia uharibifu wa mazingira na maswala
yote ya dharura yanayoweza kutokea ili kuweza kudhibiti mazingira.
Sehemu hii ina vifungu vinavyowawajibisha mameneja wa makampuni
kwa uharibifu na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kampuni
anayoiongoza.
Sehemu ya Kumi na Saba ya Muswada inatoa utaratibu wa kukata
rufaa pale inapotokea mtu hakuridhishwa na uamuzi wa Mkurugenzi Mkuu
wa Baraza au uamuzi wa Waziri. Ambaye hakuridhishwa na uamuzi wa
Mkurugenzi Mkuu anaweza kukata rufaa kwa Waziri. Asiyeridhishwa na
uamuzi wa Waziri anaweza kukata rufaa kwenye Baraza la Rufaa la
Mazingira. Sehemu hii inaelezea muundo wa Baraza la Rufaa na mamlaka
ya kisheria ya Baraza hilo.
Sehemu ya Kumi na Nane ya Muswada huu inazungumzia juu ya
kuanzishwa kwa Mfuko wa Dhamana wa Kitaifa wa Mazingira. Mfuko
huu utakapoanzishwa utatumika kutoa misaada midogo kwa vikundi vya
umma ambavyo vina programu za hifadhi ya mazingira ya kijamii na
kutolewa kwa tuzo mbalimbali za kutunza mazingira vizuri. Mfuko wa
dhamana wa mazingira umewekwa chini ya usimamizi wa Bodi ya
Wadhamini.
Sehemu ya Kumi na Tisa ya Muswada huu inaelezea vyanzo vya
mapato vya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Hifadhi ya Mazingira na uwezo wa Baraza wa kukopa na kutoa mkopo na uwezo wa kuwekeza.
Chanzo kikuu cha mapato ya Baraza kitatokana na bajeti ya serikali
inayoidhinishwa na Bunge.
Sehemu ya Ishirini ya Muswada huu inahusu mambo ya ujumla na
ya kipindi cha mpito, pia inapendekeza kufutwa kwa Sheria ya Taifa ya
Hifadhi ya Mazingira ya 1983. Pamoja na kufutwa kwa sheria
hiyo sheria hii itarithi ajira, amri na mambo yote halali yaliyofanywa au
kuamriwa katika sheria inayofutwa.
Sehemu hii pia imezungumzia malipo ya dhamana kama
mwendelezaji au mwekezaji atakayeshindwa kutekeleza masharti ya
hifadhi ya usimamizi wa mazingira. Muswada huu unatambua pia
kuendelea kutumika kwa taratibu za sasa zilizowekwa katika sheria
nyingine za maswala ya jinai na madai zinazogusa mashauri ya mazingira.
Pia sehemu hii inazungumzia maswala ya ulipwaji wa fidia kwa mtu
atakayeathirika na mazingira na unamwezesha Waziri kutengeneza kanuni
juu ya ulipwaji wa fidia hizo.
Comments
Post a Comment